Na: Khalfan Akida.
Mbunge wa jimbo la Lindi Mjini, Mhe. Hamida Abdallah ameitaka serikali kuangalia namna bora ya kuboresha viwanja vya ndege vilivyopo katika mkoa wa Lindi hususani uwanja wa Lindi na Nachingwea kutokana na umuhimu mkubwa wa viwanja hivyo katika mkoa huo.
Katika taarifa yake bungeni jijini, Dodoma leo iliyoelekezwa kwa mbunge wa Viti maalum Mkoa wa Lindi, Mhe. Tekla Ungere, Mhe. Abdallah amesema ipo haja ya serikali kuboresha viwanja vya Nachingwea na Lindi kutokana na historia kubwa iliyobebwa na viwanja hivyo kwa mkoa wa Lindi.
Aidha Mhe. Hamida ameshauri serikali kutazama namna ya kuviboresha viwanja hivyo kutokana na viwanja hivyo kurithiwa kutoka kwa serikali za wakoloni ili kulinda historia.
Awali akitoa mchango wake kwa wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, Mhe. Ungere amesema serikali iboreshe kiwanja cha ndege cha Nachingwea kutokana na kuwa kipo katikati na hivyo kuweza kutumika kama kiunganishi kutoka maeneo ya Liwale, Ruangwa na maeneo mengine mkoani Lindi.
Pia Mhe. Ungere amesema serikali inapaswa kuwekeza katika viwanja vya ndege mkoani Lindi ili kuvutia wawekezaji wanaotamani kuwekeza katika mkoa huo na hivyo kuleta maendeleo kwa watu wa Lindi.