Home BUSINESS RUVUMA WAFUNGUA SOKO LA MAHINDI,RC AOMBA WAFANYABIASHARA KWENDA KUYANUNUA KWA WAKULIMA

RUVUMA WAFUNGUA SOKO LA MAHINDI,RC AOMBA WAFANYABIASHARA KWENDA KUYANUNUA KWA WAKULIMA

 

Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Brigadia Jenerali Wilbert Ibuge kushoto,akikata utepe kuashiria ufunguzi rasmi wa soko la mahindi kwa msimu wa 2020/2021 katika kijiji cha Mgazini kata ya Kilagano Halmashauri ya wilaya ya Songea,kulia meneja wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula(NFRA)Kanda ya Songea Ramadhan Nondo.
 

Meneja wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) Kanda ya Songea Ramadhan Nondo kulia,akimounesha Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Brigadia Jenerali Wilbert Ibuge moja kati ya mizani inayotumika kupima mahindi ya wakulima katika kituo cha kununua mahindi cha Mgazini wilayani Songea.


Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Brigadia Jenerali Wilbert Ibuge,akiongea na wananchi wa kijiji cha Mgazini kata ya Kilagano katika Halmashauri ya wilaya Songea baada ya kufungua rasmi soko la mahindi kwa msimu wa mwaka 2020/2021,wa pili kushoto Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi mkoa wa Ruvuma Oddo Mwisho na kulia aliyevaa suti Meneja wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula(NFRA)Kanda ya Songea Ramadhan Nondo.

Picha zote na Muhidin Amri.

Na: Muhidin Amri,Songea.

MKUU wa mkoa wa Ruvuma Brigadia Jenerali Wilbert Ibuge, ametangaza rasmi ufunguzi wa soko la mahindi kwa wakulima wa mkoa huo yatakayonunuliwa na wakala wa Taifa wa Hifadhi ya chakula(NFRA) kanda ya Songea.

Jenerali Ibuge amesema,serikali kutokana na kuwathamini wakulima itanunua mahindi kwa bei ya Sh.500 kwa kilo, na kuwasisitiza wakulima kupeleka mahindi yenye ubora ili kuepuka usumbufu pindi wanapofikisha mahindi kwenye vituo vya kununulia mahindi.

Amesema hayo jana,wakati akifungua rasmi soko la mahindi katika kijiji cha
Mgazini kata ya Kilagano katika Halmashauri ya wilaya ya Songea.

Aidha amesema, amesema, katika msimu wa kilimo 2020/2021 mkoa huo umezalisha ziada ya mahindi tani 324,497 kati ya tani 816,242 ikilinganishwa na tani 787,321 za msimu wa mwaka 2019/2020.

“Uzalishaji huu ni zaidi ya kiwango kilichozalishwa kwa asilimia nne,ikilinganishwa na uzalishaji katika msimu uliopita ambapo ni tani 787,321 ndizo zilizozalishwa”amesema Jenerali Ibuge.

Jenerali Ibuge amesema, katika msimu wa kilimo 2020/2021 wakulima wa mahindi wameweza kulima jumla ya hekta 276,488 ambapo mkoa wa Ruvuma una uwezo wa kuuza ziada hiyo ya mahindi ndani na nje ya nchi.

Kwa mujibu wa Mkuu wa mkoa, katika awamu ya kwanza ya ununuzi wa mahindi kutakuwa na vituo tisa katika mkoa mzima ambavyo vimepangwa kwa lengo la kumrahisishia mkulima kuweza kuuza mahindi bila kutumia gharama kubwa.

Hata hivyo amesema, kiwango cha tani 32,000 kilichowekwa na NFRA katika mkoa huo ni kidogo mno ikilinganishwa na uzalishaji mkubwa uliotokana na kazi ya wakulima katika msimu wa kilimo 2020/2021.

Kutokana na hali hiyo,ameiomba Serikali kupitia wizara ya kilimo na wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula(NFRA) kuangalia uwezekano wa kuongeza mgao wa kununua mahindi ili Wakulima wa Ruvuma waendelea kujituma na kuzalisha chakula kwa wingi.

Pia Ibuge,amewakaribisha wanunuzi wengine kutoka mikoa mbalimbali hapa nchini, kufika mkoani Ruvuma kununua mahindi ili kupunguza kiasi cha ziada na iende katika mikoa na mataifa mengine yenye upungufu wa chakula ambapo amewaomba wahakikishe wananunua kwa bei nzuri ili kuleta tija kwa wakulima.

Kwa upande wake meneja wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula(NFRA)kanda ya Songea Ramadhan Nondo amesema, katika msimu wa mwaka 2020/2021 wanatarajia kununua tani za mahindi 165,000 ambapo kanda ya Songea imetengewa kununua tani 32,000 na katika awamu ya kwanza zitanunuliwa tani 6,000.

Nondo amesema, mahindi yatanunuliwa kwa bei ya Sh.500 kwa kilo katika kituo cha NFRA Songea Ruhuwiko na vituo vingine tisa yatanunuliwa kwa bei ya Sh.470.

Nondo amevitaja vituo hivyo tisa ni pamoja na Namabengo,Namtumbo mjini,Mgazini,Magagura,,Mpitimbi,,Mbinga mjini,Kigonsera na ofisi ya kanda za NFRA Ruhuwiko.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi(CCM)mkoa wa Ruvuma Oddo Mwisho, amepongeza hatua ya Serikali ya awamu ya sita kununua mahindi ya wakulima wa mkoa huo kwani uamuzi huo utachochea kuongeza uzalishaji na kuleta tija kwa wakulima.

Hata hivyo,ameiomba Serikali kuangalia uwezekano wa kuongeza kiwango cha tani za ununuzi wa zao hilo kwa sababu wakulima watauza kiasi kidogo cha mahindi ikilinganishwa na hali halisi ya uzalishaji.

“Naipongeza sana Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwa kuamua kununua mahindi ya wakulima katika mkoa wetu,lakini napenda kuishauri inunue mahindi mengi kupitia mfuko mkuu wa Serikali ili yakauzwe kwenye nchi zenye mahitaji makubwa ya chakula”amesema.

Oddo amesisitiza kuwa, wananchi wasipotafutiwa masoko ya uhakika ya mazao yao,wataendelea kupata hasara kwa kuuza kwa bei ndogo isiolingana na uzalishaji hali ambayo inaweza kuwakatisha tamaa kuendelea na kilimo cha zao la mahindi.
MWISHO.

 

 

.

 

 

Previous articleEREA YAJITAMBURISHA KWA DKT. KALEMANI
Next articleWANANCHI 2,300 WAPATA CHANJO YA UVIKO-19 RUKWA: DKT.KASULULU

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here