Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako amesema Serikali imetenga jumla ya Shilingi bilioni 48.5 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi na kununua samani za vyuo 25 vya Ufundi Stadi vya Wilaya na vinne vya ngazi ya Mkoa kupitia fedha za mpango wa maendeleo wa ustawi na mapambano dhidi ya Uviko 19.
Akizungumza wakati wa halfa ya makabidhiano na uwekaji jiwe la msingi katika Chuo cha Ufundi Stadi cha Wilaya ya Kasulu iliyofanyika Desemba 22, 2021 wilayani Kasulu amesema kuwa ukamilishaji wa vyuo hivyo utaongeza nafasi 35,600 za udahili wa wanafunzi wa ufundi stadi.
Prof. Ndalichako ameongeza kuwa kuwepo kwa vyuo hivyo kutaongeza fursa kwa vijana kupata ujuzi ambao utawawezesha kuajiriwa, kujiajiri na kuanzisha shughuli mbalimbali za kiuchumi pamoja na kushiriki katika kuimarisha uchumi wa kati kupitia viwanda.
“Leo hii kuna miradi mingi ya Serikali ambayo ina uhitaji wa vijana wenye ujuzi kufanya kazi huko, hivyo ni wakati wetu vijana kuchangamkia fursa hizi za kujiunga katika vyuo hivi vinavyojengwa nchini kote ili mpate ujuzi utakaowawezesha kujiajiri na kuajiriwa,” amefafanua Waziri Ndalichako.
Aidha, ameagiza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kuhakikisha inaharakisha mchakato wa manunuzi ya samani na vifaa vinavyopaswa kupelekwa katika vyuo hivyo vya ufundi ili kuwezesha vyuo vilivyokamilika kuanza kudahili wanafunzi mapema mwakani, huku akiwataka VETA kukamilisha ujenzi ifikiapo Juni 2022.
Mkuu wa Wilaya, Kanali Isack Mwakisu amemuhakikishia Waziri Ndalichako kuwa uongozi wa Halmashauri ya Kasulu Mjini utailinda miundombinu ya Chuo hicho ili iweze kudumu kwa muda mrefu kwa manufaa ya vizazi vijavyo vya wanaKasulu na kuwa watahamasisha vijana kujiunga ili waweze kupata ujuzi hasa wakati huu ambapo Wilaya inaanzisha eneo maalum kwa ajili ya Viwanda.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Dkt. Pancras Bujulu amesema tayari Chuo cha Wilaya ya Kasulu kimeshadahili wanafunzi 60 kwa kozi za ufundi umeme, ushonaji, useremala na ufundi wa magari, huku akitoa nafasi kwa wanafunzi 20 wa Wilaya ya Kasulu kujiunga katika chuo hicho bure.