Na: Hughes Dugilo, DAR ES SALAAM
TAKRIBANI wafanyabiashara 250 kutoka Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) wamethibitisha kushiriki Kongamano la Kimataifa la Biashara kati ya nchi za Jumuiya ya Ulaya na Tanzania na linalotarajiwa kufanyika February 23 na 24 Jijini Dar es Salaam
Mtatuzi wa Changamoto za Biashara kutoka TPSF Bi Kinanasy Seif amebainisha hayo Leo February 17 Jijini Dar es salaam kwenye mkutano wa Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Dk. Ashantu Kijaji na waandishi wa habari kuhusiana na maadlaizi ya kongamano hilo.
Alisema Taasisi hiyo imejiandaa kikamilifu kushiriki Kongamano hilo na kwamba wafanyabiashara watakao shiriki wametoka katika Sekta za kilimo, Madini, Viwanda na Biashara pamoja na Usafirishaji.
Amesema kuwa taasisi hiyo inaamini kuwa Kongamano hilo litaongeza wigo kwa wafanyabiashara kupata masoko katika soko la Ulaya kutokana na mikataba mbalimbali ya Kibiashara itakayosainiwa katika Kongamano hilo.
“Baada ya kuingia ubia tunaamini milango itakuwa imefunguka kwa bidhaa za Tanzania kuanza kuuzwa kwenye soko la Ulaya, na hiyo itasaidia kukua kwa uchumi wetu kutokana na uzalishaji kuongezeka na soko la ajira litakua” amesema Kinanasy.
Aidha ameishukuru Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji nchini na kuweka mazingira wezeshi ya ufanyaji Biashara hapa nchini.
TPSF ikiwa kama Injini ya uchumi inashiriki Kongamano hilo linalofanyika kwa mara ya kwanza nchini Tanzania kama mdau mkubwa wa Sekta Binafsi huku ikiwa na matumaini makubwa ya Kongamano hilo litaongeza fursa kwa wafanyabiashara wa Tanzania.
Mwisho.