Wanafunzi na Naibu Waziri – Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Mwanaidi Ali Khamis (wa kwanza kutoka upande wa kulia) akiwapa Taarifa ya Utafiti kuhusu Hali ya Ukatili dhidi ya Watoto Mtandaoni Wawakilishi kutoka Baraza la Taifa la Watoto.
Baadhi ya washiriki kutoka taasisi mbalimbali wakiwa katika uzinduzi wa Taarifa ya Utafiti kuhusu Hali ya Ukatili dhidi ya Watoto mtandaoni uliofanyika leo tarehe 18/3/2022 jijini Dar es Salaam
Serikali imetaka jamii kuwa utamaduni wa karibu na watoto katika kuhakikisha wanapata malezi bora, kuwazui na matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii jambo ambalo litasaidia kuwaepusha na ukatili dhidi ya watoto mtandaoni.
Akizungumza jana tarehe 18/3/2022 jijini Dar es Salaam wakati akizindua Taarifa ya Utafiti kuhusu Hali ya Ukatili dhidi ya Watoto Mtandaoni, Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Mwanaidi Ali Khamis, alisema kuwa serikali itaendelea kuimarisha mifumo yote ya ulinzi kama ilivyoelekezwa katika mikataba ya kikanda na kimataifa kuhusu haki na ustawi wa mtoto ili kumlinda na vitendo vya ukatili mtandaoni.
“Tutaendelea kusimamia sera na sheria mbalimbali zinazo muhusu mtoto na kuandaa miongozo inayohitajika ili kuhakikisha hakuna mtoto anayefanyiwa ukatili mtandaoni “alisema Mhe. Mwanaidi.
Alisema kuwa amefarijika kupata taarifa ya hali ya ukatili wa mtandaoni katika kipindi hiki, kwani awali ameanza kushuhudia watoto wakipata madhara yanayotokana na ukatili wa mtandaoni hapa nchini.
“Katika siku za hivi karibuni tumeshuhudia matumizi makubwa ya vifaa vya kielektroniki hasa baada ya mlipuko wa ugonjwa wa UVIKO 19, ambapo vifaa hivyo vimekuwa kiungo muhimu kwa ajili ya mawasiliano kwenye kuendesha vikao mbalimbali” alisema Mhe. Mwanaidi.
Alieleza kuwa taarifa ya utafiti wa ukatili dhidi ya watoto mtandaoni uliofanyika mwaka 2018 na Mtaalam kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dkt Hezron Onditi umeonyesha asilimia nne ya watoto wenye umri kati ya miaka 12 hadi 17 walifanyiwa ukatili wa kingono ikiwemo kulazimishwa kutoa picha zao za utupu.
“Pamoja na faida nyingi katika nyanja za kiuchumi, kijamii na kisiasa, tumeshuhudia matumizi yasiyo sahihi ya mitandao ya kijamii yakihusisha zaidi kundi la watoto na vijana balehe” alisema Mhe. Mwanaidi.
Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Mtoto Bw. Sebastian Kitiku, alisema kuwa matumizi ya vifaa vya kielekroniki vimekuwa vikitumika kwa wingi, hivyo kumekuwa na changamoto ya kutaka kujua ukubwa wa tatizo hilo, hivyo serikali kwa kishirikiana na wadau wakaona ni vyema kufanya utafiti.
“Utafiti umetumia mbinu mbalimbali kama uchambuzi wa sera na sheria zilizopo nchini, upitiaji wa nyaraka mbalimbali mitandaoni, mahojiana na watoto na wazazi pamoja na mikusanyiko mbalimbali kwa kushirikiana na uongozi wa ngazi za Kata hadi Mkoa.”alisema Bw. Kitiku
Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Watoto Nancy Kasembo, alishukuru kwa kushirikishwa watoto katika michakato wa utafiti, kwani ina manufaa kwao na kuiomba jamii kutoa taarifa za vitendo vya ukatili kwa watoto katika mamlaka husika ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa kwa wakati.
“Watoto hawajui namna ya kutoa taarifa baada ya kufanyiwa ukatili, aidha bado kuna unyanyapaa dhidi ya wahanga wa ukatili na kusababisha wahanga kutotoa taarifa” alisema Nancy.
Mwakilishi Mkazi wa Shirika la UNICEF Bi. Shalini Bahguna, aliipongeza Serikali kwa kuweka juhudi za msingi kupinga ukatili dhidi ya wanawake na watoto hasa katika jitihada za kupambana na ukatili mtandaoni.
Alisema Shirika hilo limejikita katika kuhakikisha watoto wapo katika mazingira salama na wanajengewa uwezo wa kujitambua ili kuepukana na ukatili wa mtandaoni.
Alieleza kuwa serikali inatakiwa kuendelea kutoa ushirikiano kwa taasisi mbalimbali katika kupinga ukatili wa watoto mtandaoni.
“Wadau mbalimbali wanatakiwa kuongeza wigo katika kutoa mafunzo ili kuzuia watoto kutumia mitandao ya kijamii na matumzi mabaya ya mtandaoni hapa nchini” alisema.
Alifafanua kuwa suala la ukatili la watoto mtandaoni lipewe kipaombele ili kutokomeza ukatili huo pamoja na kuangalia namna ya kuongeza nguvu katika kupinga.
Baadhi ya wadau wakichangia umuhimu wa utafiti huo, walisema ni vyema kuwekeza katika kuzuia watoto kufanyiwa ukatili wa mtandaoni kabla haujatokea.
Waliiomba serikali kuwajengea uwezo watoa huduma katika madawati ya kijinsia ili waweze kutoa elimu kwa wazazi na walezi kwa kuwajengea ukaribu wa watoto waweze kusema pale wanapofanyiwa ukatili.
Credit – Fullshangwe Blog.