BALOZI wa Ufaransa nchini Tanzania Nabil Hajlaoui pamoja na Babalozi wengine wa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya (EU) amezungumzia mapigano yanayoendelea kati ya Ukraine na Urusi katika kuhakikisha amani inarejea katika nchi hizo kwa njia ya mazungumzo ili kuepuasha madhara zaidi yasiendelee kutokea.
Balozi Hajlaoui ameyasema hayo Machi 22,2022 alipokutana na waandishi wa habari akiwa pamoja na Mabalozi wa nchi wanachama wa Umoja huo katika makazi yake yaliyopo katika Ubalozi wa Ufaransa JIjini Dar es Salaam.
Ameeleza kuwa Ufaransa na nchi zilizopo katika Umoja huo wanasimama na Ukraine kuhakikisha vita hiyo inamalizika na nchi hizo mbili kukaa pamoja kufanya mazungumzo ya amani na kwamba jitihada ni katika kuhakikisha hakuna madhara zaidi yatakayoweza kutokea.
Aidha Balozi Hajlaoui amesema kuwa mnamo Machi 2,2022 Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipitisha azimio linaloitaka Urusi kusitisha mara moja matumizi ya nguvu dhidi ya Ukraine katika kura iliyoidhinishwa kwa wingi na nchi 141 ikiwa ni pamoja na nchi zote wanachama wa Umoja wa Ulaya huku nchi tano zikipinga na nchi 35 kuacha kupiga kura Kati ya wanachama 193 wa Jumuiya.
“Urusi imeanzisha vita bila uchokozi wowote na ukiukwaji mkubwa wa sheria za Kimataifa na ahadi zake zote,nchi 27 wanachama wa EU zimepitisha vikwazo vikubwa dhidi ya Urusi . Jumuiya inasikitishwa na matumizi makubwa ya nguvu yanayotumika kuishambulia Ukraine,”amesema Balozi Hajlaoui.
Ameongeza kuwa EU imeamua kuweka vikwazo vya moja kwa moja kwa watu wanaohusika na maamuzi yanayohusiana na vita lakini pia mfumo wa kiuchumi wa umma na wa kibinafsi wa Urusi ambao unaunga mkono juhudi hizo za vita na kwamba katika upande wa kifedha Urusi iko karibu kuondolewa kwenye masoko ya kifedha.
“Vikwazo hivyo pia vitakuwepo katika kuzuia Uwekezaji wote katika sekta ya nishati ya Urusi na utangazaji wa vyombo vya habari ambavyo vinarudisha propaganda za vita vya Urusi katika EU. Tayari vikwazo hivyo vimeanza kufanya kazi,”ameongeza Balozi Hajlaoui.
Aidha amesema kuwa EU iko tayari kuongeza shinikizo zaidi ili kuongeza ukali wa vita kwa Urusi na kuifanya nchi hiyo kuamua kusitisha mapigano na kufikia mazungumzo kama Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alivyotangaza katika mkutano wa wakuu wa nchi za Ulaya wa Versailles Machi 10-11 mwaka huu.
Katika taarifa ya pamoja ya Ufaransa na EU inaeleza kuwa wanachama wa Umoja huo wanaunga mkono kufunguliwa kwa uchunguzi wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai katika mashambulizi ya Urusi na kusababisha madhahara makubwa kwa Raia wakiwemo majeruhi.
“Hata hivyo Rais Emmanuel Macron anaendelea na mazungumzo na Vladimir Putin ili kupata suluhisho la amani katika mgogoro huo” inaeleza taarifa hiyo.
katika hatua nyingine Balozi Nabil pamoja na Umoja wa Ulaya wametoa ombi kwa nchi za Afrika ikiwemo Tanzania kutoa kauli kwa Urusi ili iwezeshe kusitisha vita dhidi ya Ukraine na kwamba nchi za Afrika zinatambua madhara yanayopatikana kutokana na vita hiyo.