Meneja Mradi wa giZ Faustine Msangira (kulia) akiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa TWCC Mwajuma Hamza (Kushoto) wakiangalia bidhaa zilizofungashwa katika ubora wa hali ya juu kutoka kwa mjasiriamali mwananchama wa TWCC katika maonesho ya Bidhaa za Viwanda yanayoendelea kwenye viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere (Sabasaba) Jijini Dar es Salaam.
Meneja Mradi wa giZ Faustine Msangira (kulia) akiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa TWCC Mwajuma Hamza (Kushoto) wakipata maelezo kutoka kwa Mjasiriamali anayezalisha bidhaa za nguo katika maonesho ya Bidhaa za Viwanda yanayoendelea kwenye viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere (Sabasaba) Jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa TWCC Mwajuma Hamza (Kulia) akisikiliza maelezo kutoka kwa mjasiriamali anayezalisha bidhaa za nguo katika maonesho hayo yanayofanyika Jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa TWCC Mwajuma Hamza (wa kwanza Kulia) akiwa na mgeni wake Meneja Mradi wa giZ Faustine Msangira (wa pili kulia) katika banda la wajasiriamali kutoka Wilaya ya Mwanga Mkoani Kilimanjaro katika Maonesho hayo.
Meneja Mradi wa giZ Faustine Msangira (kushoto) akiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa TWCC Mwajuma Hamza (kulia) akifurahia jambo na Meneja huyo kukamilisha ziara yake fupi ya kutembelea mabanda ya wajasiriamali hao.
Meneja Mradi wa giZ Faustine Msangira akitia saini katika kitabu cha wageni katika Banda la TWCC mara baada ya kutembelea Mabanda ya wajasiriamali kujionea na kufurahia ubora wa Bidhaa za wajasiriamali hao.
Na: Hughes Dugilo, Dar es Salaam.
Meneja Mradi wa giZ Faustine Msangira amepongeza ubora wa Bidhaa zinazozalishwa na wajasiriamali wa Chama cha Wafanyabiashara wanawake Tanzania (TWCC) wanaoshiriki katika Maonesho ya saba ya Bidhaa za viwanda vya Tanzania yanayofanyika katika viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam.
Msangira ametoa pongezi hizo alipokuwa akitembelea Mabanda ya Wajasiriamali hao kujionea bidhaa wanazozalisha na kusema kuwa ipo haja ya kupongeza kazi nzuri inayofanywa na wajasiriamali hao na kuwaunga mkono.
Katika ziara yake yake Kiongozi huyo aliongozana na Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Wafanyabiashara Wanawake Tanzania (TWCC) Mwajuma Hamza aliyekuwa akitoa utambulisho kwa mjasiriamali mmoja mmoja pamoja na bidhaa alizokuwa nazo.
Aidha Mwajuma amebainisha kuwa zaidi ya wajasiriamali 100 kutoka katika mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara na Visiwani wameshiriki katika Maonesho hayo.
“Haya ni Maonesho maalumu kwaajili ya kuonesha bidhaa zetu zinazozalishwa na wajasiriamali wetu wa hapa nchini, hii ni fursa kubwa kwao kuonesha kile wanachokifanya na sisi TWCC tumekuja na wajasiriamali zaidi ya 100 hapa ambao wamepata fursa ya kuonesha Bidhaa zao na kukutana na wadau wengine kubadilishana uzoefu na kupanua wigo wa masoko yao” amesema Mwajuma.