Home BUSINESS SERIKALI YALENGA KUONGEZA MAPATO YASIYO YA KODI KUTOKA KWA MASHIRIKA YA UMMA 

SERIKALI YALENGA KUONGEZA MAPATO YASIYO YA KODI KUTOKA KWA MASHIRIKA YA UMMA 

Thank you for reading this post, don't forget to subscribe!

Na: mwandishi wa OMH

Dodoma. Rais wa Tanzania Mhe. Dk. Samia Suluhu Hassan amesema Serikali itafanya mageuzi ya mashirika ya umma ili kuboresha ufanisi, uwazi na tija.

Akihutubia Bunge la Tanzania Ijumaa, Novemba 14,2025, Mhe. Rais alisema serikali inataka kuongeza sio tu gawio ambalo Serikali inapokea, lakini pia kufikia lengo la Mashirika na Taasisi za Umma kuchangia angalau asilimia 10 ya mapato yote yasiyo ya kodi.

Alisema mageuzi hayo ni sehemu ya jitihada za Serikali kuimarisha mashirika ya umma na kuyawezesha kushindana kibiashara katika soko la kimataifa.

“Nia yetu ni kuyajengea uwezo Mashirika ya Umma yaweze kushindana na kuwekeza nje ya Tanzania, kama mashirika mengine ya nje tunavyoyaona hapa nchini kwetu,” alisisitiza.

Aliongeza: Mageuzi haya ni sehemu ya mchakato mpana wa kitaifa wa kuimarisha sekta za umma na kuweka msingi madhubuti wa uchumi, unaolenga kufanikisha malengo ya Taifa kufikia mwaka 2030.”

Akifafanua zaidi kuhusu msingi wa mageuzi hayo, Rais Samia alisema ili kuimarisha uwajibikaji Serikalini, Serikali itaendelea kutekeleza programu za maboresho ya utumishi wa umma, ikiwemo matumizi ya mifumo ya upimaji wa utendaji kazi.

Alibainisha kuwa wajibu huenda na haki, au haki huambatana na wajibu, na hivyo pamoja na kuwataka watumishi wa umma kuwajibika ipasavyo, Serikali itaendelea kuboresha maslahi yao kadri uchumi utakavyoruhusu.

Ikumbukwe kuwa mashirika ya umma yako chini ya uangalizi wa Ofisi ya Msajili wa Hazina, hivyo ndio yenye jukumu la kuhakikisha utendaji wake unazingatia uwajibikaji na ufanisi.

Katika muktadha huo, Msajili wa Hazina, Bw. Nehemiah Mchechu, amesema maagizo ya Mhe. Rais yamepokelewa na kwa sasa yanaendelea kutafsiriwa kupitia mikakati na mipango ya ofisi, hatua ambayo inalenga kuhakikisha utekelezaji wake unaleta matokeo chanya.

Tanzania ina mashirika na taasisi za umma zinazoendesha huduma muhimu za kijamii, viwanda na sekta ya kifedha, zikiwemo benki, viwanda vya umeme na mashirika ya usafirishaji.

“Ofisi ya Msajili wa Hazina inaendelea na jitihada za kuhakikisha changamoto za kiutendaji—ikiwemo ufanisi mdogo kwa baadhi ya taasisi na changamoto za mitaji zinatatuliwa,” alisema Bw. Mchechu.