Home BUSINESS MIVUTANO YA MADIWANI YACHELEWESHA AHADI YA DKT.SAMIA UJENZI WA SOKO LAMADI

MIVUTANO YA MADIWANI YACHELEWESHA AHADI YA DKT.SAMIA UJENZI WA SOKO LAMADI

Thank you for reading this post, don't forget to subscribe!

Mgombea wa Nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema kutotekelezwa kwa ahadi yake ya Ujenzi wa soko Lamadi Wilayani Busega Mkoani Simiyu kumetokana na mivutano ya Baraza la Madiwani la Halmashauri hiyo, waliokuwa wakivutana kutaka kubadilisha eneo la ujenzi wa soko hilo kama ilivyokuwa ahadi yake wakati alipofanya ziara eneo hilo.

Dkt. Samia ameyasema hayo leo Alhamisi Oktoba 09, 2025 akiwa kwenye Mkutano wake wa Kampeni kwenye Viwanja vya Kituo cha Mabasi Lamadi na kuagiza kuwa ni muhimu soko hilo likajengwa sehemu aliyoahidi na ikiwa Madiwani wanataka soko hilo lijengwe Nyashimo, basi yatumwe maombi mengine ya kutaka soko huko.

“Niliahidi na kama mnavyojua Samia Suluhu akiahidi anatekeleza, nilitenga fedha za kujenga soko hapa Lamadi lakini ni Uongozi wa Halmashauri (Madiwani) wanabishana Lamadi au Nyashimo. Soko lile halikujengwa lakini ahadi yangu ipo palepale, Madiwani watakapoelewana litajengwa na ahadi yangu wakati ule ilikuwa ni soko lijengwe Lamadi kama kuna mahitaji ya soko Nyashimo hilo ni ombi lingine.” Amekaririwa akisema Dkt. Samia.

Kulingana na Dkt. Samia soko hilo pamoja na ujenzi wa Kituo cha mabasi Nyashimo vitatekelezwa chini ya Mradi wa uendelezaji Miji Tanzania maarufu kama TACTIC, Akisema mara baada ya Madiwani kukubaliana, mradi huo utaanza kutekelezwa kwani fedha tayari zimetengwa.

Dkt. Samia pia ameeleza mafanikio makubwa ya utekelezaji wa Ilani ya mwaka 2020/25 ya Chama chake, akiomba kura kwa wananchi wa eneo hilo na kusema Chama Cha Mapinduzi ni muhimu kikachaguliwa kwasababu kinawafahamu vyema wananchi wa Lamadi, kikiwa na uzoefu na masuala ya Uongozi wa serikali tofauti na Vyama vingine ambavyo vitataka muda mkubwa wa kujifunza na kujua fedha zinapopatikana ili kutekeleza miradi ya maendeleo.