Na Mwandishi Wetu, Pemba
WANANCHI wa shehia za Majenzi, Chamboni, Micheweni, Shumba mjini na Mjini wingwi wilaya ya Micheweni Pemba, wamekumbushwa kuzirasimisha ardhi zao, mara baada ya kuzimiliki, ili kujiepusha na migogoro isiyokuwa ya lazima.
Ushauri huo umetolewa leo Juni 1, 2025 na Mkuu wa Idara ya Upimaji na Ramani Pemba, Salim Khamis Haji, alipokuwa akizungumza na wananchi hao, kwenye muendelezo wa kampeni ya kitaifa ya msaada wa kisheria ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mkutano uliofanyika skuli ya Micheweni.
Alisema, migogoro kadhaa hujitokeza, kwa wananchi waliowengi kushindwa kuzirasimisha ardhi zao, katika taasisi husika, na kusababisha siuntafahamu baina ya pande moja na nyingine.
Alieleza kuwa, njia za kumiliki ardhi kisheria zipo tano ikiwemo kununua, kupewa na serikali, kuvunja pori, kurithi pamoja na kupewa zawadi ingawa kisha kinachofuata ni kuzirasimisha na kupata hati za matumizi.
‘’Niwanasihi wananchi wenzangu wa wilaya ya Micheweni, kufanya haraka mara mnapokuwa na ardhi, mhakikishe mnazirasimisha, ili ziongezeke thamani,’’ alifafanua.
Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa Idara, aliwakumbusha wananchi hao, kuzitumia siku tisa za kampeni hiyo, kujifunza mambo kadhaa ya kisheria, ili kujua haki na wajibu wao.
Kwa upande wake Kadhi wa wilaya ya Micheweni sheikh Mansabu Khamis Omar, amewataka wazazi na walezi, kusimamia haki ya mahari ya watoto wao, kabla ya ndoa kuvunjika.
Alieleza kuwa, kumekuwa na wimbi kubwa la vijana kulalamikia juu ya kutomaliziwa mahari yao, jambo ambalo husababisha mifarakano kwa wanandoa na familia zao.
‘’Wazazi tunaowajibu wa kuhakikisha, watoto wetu wamaliziwa mahari yao, maana wanapokuja mahakamani kulalamikiana juu ya kesi zao, na haki ya mahari huitaja,’’ alifafanua.
Mapema Afisa sheria kutoka Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana Pemba, Massoud Ali Massoud aliwakumbusha wananchi, kurithi mali za marehemu mapema, ili kuepusha migogoro inayozuilika.
Alieleza kuwa, tayari dini ya kiislamu imeshaelekeza kuwa, miongoni mwa mambo ambayo yanastahili kufanywa haraka, baada ya mtu kufariki pamoja na urithi.
Baadhi ya wananchi wa shehia hizo, wamesema ujio wa wataalamu hao wa sheria, umesaidia kupata ufafanuzi wa masuala kadhaa waliokuwa wamekwama.
Mohamed Shamata Kombo, alisema sasa amepata ufafanuzi wa kesi yake ya ardhi, baada ya kukutana na mtaalamu kutoka Idara ya ramani na upimaji.
Nae Hidaya Mjaka Kassim na Halima Mzee Othman, walisema sasa wamepata mwelekeo wa kulipata shamba la eka, ambalo walikuwa hawajui wafanye nini baada ya wazazi wao kufariki.
Zaidi ya wananchi 237 wamejitokeza na kupewa elimu, ushauri na msaada wa kisheria kutoka katika shehia hizo tano, kwenye muendelezo wa kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia.