Na Hughes Dugilo -IRINGA
TUME ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC), imepiga hatua kubwa katika utekelezaji miradi yake nchini, ambapo katika kipindi cha uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan jumla ya miradi 783 inasimamiwa huku miradi 125 kati ya hiyo wakandarasi wapo kazini.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa NIRC, Edmund Mndolwa, katika kikao kazi kati ya Tume hiyo na Wahariri wa vyombo vya habari, kuhusu mafanikio ya Sekta ya Umwagiliaji katika kipindi cha uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita uliofanyika leo Juni 24, 2025 Mkoani Iringa.
Amesema kuwa miradi hiyo ina thamani ya jumla ya Shilingi Trilioni 1.2, na kwamba Tume imeendelea kutekeleza malengo yake katika sekta ya umwagiliaji kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo katika sekta hiyo.
“Tume imeendelea kufanya ukarabati wa miundombinu ya umwagiliaji iliyoharibika na isiyofanya kazi, sambamba na kuendelea na ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji katika skimu mpya za umwagiliaji, pamoja na ujenzi wa mabwawa mapya ya kuvunia maji ya mvua kwa ajili ya shughuli za kilimo cha umwagiliaji nchini.” amesema Mndolwa.
Aidha, amesema Tume imeendelea kuimarisha usimamizi wa shughuli za umwagiliaji kwa kufungua ofisi 121 za wilaya, kuajiri watumishi 340, kununua magari 58, mitambo 30 kwa ajili ya ujenzi, pamoja na kununuua magari makubwa 17 na mitambo 17 ya kuchimba visima 10 vya umwagiliaji.
Sambamba na hilo, ame kuna ongezeko la eneo linalomwagiliwa kutoka hekta 461,000 mwaka 2014/2015 hadi hekta 983,466.06 mwaka 2024/25, pamoja na ongezeko la miradi inayosanifiwa na inayoendelea kusanifiwa kutoka miradi 10 mwaka 2021/2022 hadi zaidi ya miradi 655 mwaka 2024/2025.
Katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, Mndolwa ameongeza kuwa, Tume hiyo inahakikisha upatikanaji wa maji kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji kwa kujenga mabwawa, kuchimba visima, na ujenzi wa miundombinu katika mabonde 22 ya kimkakati.
“Kutokana na ongezeko hilo la eneo la umwagiliaji, tija katika mazao mbalimbali kakiemon mpunga, mahindi, vitunguu na nyanya imeongezeka kutoka tani 1.8 hadi 2.0 kwa hekta na kufikia wastani wa tani 5.0 hadi 8.0 kwa hekta, tani 1.5 hadi tani 3.7 hadi 5.0, tani 13 hadi 26, na tani 5 hadi 18 kwa hekta mtawalia,” amesema
Katika hatua nyingine, Tume hiyo inatarajia kufanya ziara kwa Wahariri na waandishi wa habari, kutembelea mradi wake wa umwagiliaji Mkombozi, uliopo tarafa ya Pawaga, Kata ya Mboliboli na Itunundu, Wilayani Iringa ili kuona hali ya utelezaji wa mradi huo.
Mwisho