Home LOCAL TAASISI ZA UMMA ZATAKIWA KUTUMIA MIFUMO YA TEHAMA KURAHISISHA UTOAJI HUDUMA

TAASISI ZA UMMA ZATAKIWA KUTUMIA MIFUMO YA TEHAMA KURAHISISHA UTOAJI HUDUMA

Thank you for reading this post, don't forget to subscribe!

DODOMA 

Taasisi na Mashirika ya Umma nchini, zimetakiwa kutumia kikamilifu mifumo ya TEHAMA ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi.

Rai hiyo  imetolewa Juni 17,2025 na WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais  Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene, wakati wa uzinduzi wa Wiki ya Utumishi wa Umma inayofanyika katika Viwanja vya Chinangali Jijini Dodoma.

Waziri huyo amesema kuwa Mfumo huo umeletwa kwa nia njema ya kurahisisha huduma na kuhakikisha kuwa wananchi wanapata huduma bila kulazimika kuzifuata ofisi mahali zilipo, nakwamba Taasisi  ambazo bado hazijajiunga kwenye mfumo huo zichukue hatua ya kujiunga mara moja. 

“Hadi sasa ni Taasisi 185 pekee ndizo ambazo tayari zimeunganishwa kwenye mfumo huo unaowezesha huduma kutolewa kwa urahisi na kwa pamoja, na kupunguza adha kwa wananchi” amesema Simbachawene 

Aidha, amebainisha kuwa mfumo huo unahakikisha huduma za Serikali zinaingiliana na kurahisisha wananchi kupata huduma kwenye kituo kimoja na kuokoa muda.

Moja ya Taasisi zinazoshiriki Maonesho hayo, ni Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), linalotekeleza miradi mbalimbali ya ujenzi wa nyumba za makazi na miradi ya biashara nchi nzima.

Katika Maonesho hayo NHC imejielekeza katika kutoa elimu kwa wananchi kufahamu shughuli mbalimbali za Shirika, sambamba na kuelezea namna wanavyotekeleza miradi yao, ili kutoa fursa kwa wananchi hao kushiriki katika umiliki wa nyumba na maeneo ya biashara katika miradi hiyo.

Miradi hiyo ni pamoja na Nyumba za Medeli na  iyuumbu zilizopo Dodoma, ambazo zimekuwa kivutio kikubwa kwa wananchi wanaotembelea banda la NHC katika Maonesho hayo yanayofanyika kwenye viwanja vya  Chinangali Park Jijini humo.

Wiki ya Utumishi wa Umma ni jukwaa linalozileta pamoja Taasisi mbalimbali za Serikali na kutoa fursa kwa wananchi kutembelea, kujifunza na kupata huduma za papo kwa hapo,  ambapo jumla ya Taasisi 120 zimeshiriki.