Home BUSINESS RAIS SAMIA AYATAKA MASHIRIKA YA UMMA KUENDELEZA UWEKEZAJI KWENYE TAASISI ZAO

RAIS SAMIA AYATAKA MASHIRIKA YA UMMA KUENDELEZA UWEKEZAJI KWENYE TAASISI ZAO

Thank you for reading this post, don't forget to subscribe!

Dar es Salaam

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa wito  kwa Mashirika na Taasisi za Umma kuhakikisha yanawajibika ipasavyo katika kulinda na  kuendeleza uwekezaji wa Serikali kwenye mashirika hayo, na kuchangia kikamilifu  kwenye maendeleo ya kiuchumi. 

Rais Dkt. Samia ametoa wito huo leo katika hafla ya kupokea gawio na michango kutoka  kwa Taasisi na Mashirika ya Umma na Kampuni ambazo Serikali ina hisa.  

Katika hotuba yake, Rais Dkt. Samia amesema kuwa mageuzi makubwa yanayotekelezwa na Serikali kwenye usimamizi na uendeshaji wa Mashirika ya Umma yameanza kuonesha  mafanikio, ikiwemo Mashirika 11 kati ya 13 yaliyokuwa na mtaji hasi kuhamia kwenye  kundi lenye mtaji chanya, na Mashirika mengine nane katika hayo yaliyokuwa yanapata  hasara sasa yameanza kupata faida. 

Katika kuzidi kuongeza mchango wa Mashirika kwenye uchumi, Rais Dkt. Samia  amemuagiza Msajili wa Hazina, Bw. Nehemiah Mchechu kuendelea kuwajengea uwezo  watendaji na kuhakikisha mashirika yanaongeza ubunifu na kuimarisha matumizi ya  TEHAMA.  

Vilevile, amemtaka Msajili wa Hazina kufanya tathmini ya kuangalia namna ya kuongeza  ushiriki wa wananchi katika umiliki wa mashirika kupitia soko la hisa. 

Rais Dkt. Samia pia amesisitiza umuhimu wa kutambua Mashirika na Taasisi ambazo  hazitoi mchango wa fedha moja kwa moja kwa Serikali, bali huchangia kupitia kuboresha  utoaji huduma kwa wananchi. 

Serikali imepokea gawio la jumla ya Shilingi Trilioni 1.028 kutoka katika Mashirika na  Taasisi za Umma ikiwa ni ongezeko la asilimia 34 ikilinganishwa na Shilingi Bilioni 767  zilizotolewa mwaka jana.  

Aidha, idadi ya Mashirika na Taasisi zilizochangia imeongeza kufikia 213, huku kampuni  zenye hisa chache za Serikali zikiwa miongoni mwa wachangiaji wakubwa, zikiwemo Twiga Minerals (Shilingi Bilioni 93.6), Airtel Tanzania (Shilingi Bilioni 73.9) na NMB Bank  (Shilingi Bilioni 68.1).  

Shaaban Kissu 

Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu