Home BUSINESS NGOME YA JESHI LA UJERUMANI KIVUTIO KIPYA CHA UTALII WA NDANI SERENGETI

NGOME YA JESHI LA UJERUMANI KIVUTIO KIPYA CHA UTALII WA NDANI SERENGETI

Na Mwandishi Wetu

Thank you for reading this post, don't forget to subscribe!

Ngome ya Jeshi ya zamani maarufu kwa Jina la Fort Ikoma iliyopo ndani ya Hifadhi ya Taifa Serengeti, imetajwa kuwa eneo la kipekee linalovutia watalii ndani ya hifadhi hiyo na tasnia ya utalii nchini likiunganisha historia na asili, huku watanzania wakihimizwa kufanya utalii wa ndani ili kujifunza na kufurahia utajiri wa rasilimali za taifa.

Afisa Mahusiano ya Jamii wa Hifadhi ya Taifa Serengeti, Abed Mwesigwa amebainisha hayo ndani ya eneo hilo alipokuwa akieleza kuhusu utajiri wa historia na rasilimali zilizopo ndani ya hifadhi hiyo mbele ya waandishi wa habari waliofanya ziara hifadhini hapo jana.

Mwesigwa amesema: “Mtalii yeyote akifika Serengeti bila kutembelea Fort Ikoma atakuwa amekosa kupata utajiri wa historia na asili kwani eneo hilo ndipo asili inayojumuisha wanyamapori na ekolojia ya hifadhi zinakutanishwa na historia ya ngome hiyo yenye masimulizi ya kusisimua.”

Mwesigwa amebainisha kwamba, Fort Ikoma ilijengwa na wakoloni Wajerumani mwaka 1905, ikiwa ngome yao ya kijeshi wakati ikiitawala Tanzania Bara (Tanganyika), ikiwa katika pembe ya Kaskazini Magharibi ya hifadhi maarufu duniani ya Serengeti iliyo chini ya Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA), iliyobeba tuzo za kimataifa za ubora duniani kwa miaka sita mfululizo ya European Award for Quality Choice Achievement 2025.

“Ukidhani Serengeti ni simba, nyumbu na uwanda usio na mwisho pekee, fikiria tena na uje kuishuhudia Fort Ikoma na kujua historia yake. Kukosa kuitembelea ni sawa na kusoma riwaya ya kusisimua kwa kuiruka sura ya kwanza,” amesema Mwesigwa.

Waandishi wa Habari waliotembelea Hifadhi ya Taifa Serengeti, inayoshikilia tuzo ya Hifadhi Bora Afrika kwa miaka mitano mfululizo mwaka 2019 -2023, waliishuhudia Fort Ikoma, majengo yake yaliyojengwa kwa mawe na kuwekwa nakshi zinazovutia licha ya kujengwa zaidi ya miaka mia moja iliyopita.  

Kwa mujibu wa Mwesigwa, jengo hilo ni ishara ya nguvu na utawala wa Ujerumani kwa wakati huo, likiwa kwenye muinuko wa juu, uliowawezesha kuona maadui kwa mbali kutoka pande zote, hivyo kujihami kwa urahisi huku historia ikionyesha, Wajerumani walinyang’anywa koloni lao Tanganyika na kupewa Uingereza, baada ya Vita Kuu ya Dunia mwaka1914 – 1918, hivyo Fort Ikoma ikawa mikononi mwa Uingereza. 

“Leo, watalii wanaweza kutembelea magofu hayo, kutembea katika mapango yake yenye hadithi ya kusisimua na kujiwekea picha ya wanajeshi, viongozi na jamii za wenyeji waliowahi kuipa uhai ngome hiyo iliyojaa matundu ya risasi.” amesema Mwesigwa na kuongeza: Fort Ikoma ipo katikati ya mfumo wa ikolojia wa Serengeti, hivyo ni mahali bora pa kushuhudia uhamaji wa wanyama, kuona wawindaji wakifanya yao na kufurahia machweo ya jua yanayoangaza savanna na kuta za kale kwa mwanga wa dhahabu.

Mwesigwa anasema kuwa baada ya kupata uhuru mwaka 1961, Serikali chini ya Rais wa kwanza na mwasisi wa Tanzania, Hayati Mwalimu Julius Nyerere ililitwaa eneo hilo kutoka kwa Wakoloni wa Uingereza na kulifanya kuwa kambi ya Jeshi la Wananchi (JWTZ).

Hata hivyo, Mwesigwa ameeleza kwamba mwaka 1997, Serikali ilifanya uamuzi mkubwa wa mabadiliko, ambapo ikaliweka eneo la Fort Ikoma kuwa chini ya Mamlaka ya Hifadhi za Taifa. (TANAPA), ikiwa sehemu ya Hifadhi ya Taifa Serengeti, pia Ofisi Kuu ya Uhusiano na Jamii.

“Serikali iliona Fort Ikoma isingeendelea kuwa kambi ya kijeshi, bali kuwa sehemu ya mtandao wa Hifadhi za Taifa (TANAPA), hivyo ikaingizwa rasmi ndani ya mipaka ya Hifadhi ya Serengeti. Tangu wakati huo, Fort Ikoma imeibuka si tu kama kivutio cha kihistoria, urithi wa utalii na daraja kati ya historia,wanyamapori na uoto wa asili.

Mwesigwa amesema msafiri anayependa kutembelea Fort Ikoma siyo tu kituo cha kupita bali sehemu ya kupata ujumbe, ukumbusho kuwa Serengeti siyo safari tu ya kuona Wanyama bali ni jumba la makumbusho hai la historia, mapambano na mabadiliko.