Home BUSINESS MCL YAKWAA KISIKI KESI YA MCHECHU, MAHAKAMA YA RUFANI YABARIKI ALIPWE FIDIA...

MCL YAKWAA KISIKI KESI YA MCHECHU, MAHAKAMA YA RUFANI YABARIKI ALIPWE FIDIA YA BIL 2.5

Thank you for reading this post, don't forget to subscribe!

Dar es Salaam

Mahakama ya Rufani leo tarehe 4 June 2025, imetupilia mbali maombi ya rufani namba 658 ya 2023 yaliyofunguliwa na kampuni ya Mwananchi communication (MCL), yaliyomhusisha Mhariri na Gazeti la The Citizen dhidi ya Nehemia Kyando Mchechu.

Mahalama hiyo imekukubaliana na uamuzi wa Mahakama kuu kwenye kesi Namba 48 ya mwaka 2021 kati ya Mwananchi communication ikimuhusisha Mhariri na Gazeti la The Citizen, dhidi ya Nehemia Kyando Mchechu uliosomwa tarehe 3 Machi, 2023 mbele ya Jaji Leila Mgonya.

Katika uamuzi huo wa mahakama ya rufani uliotolewa na Majaji watatu, akiwemo Jaji Mhe. Rehema Kerefu, Jaji Omar Othman Makungu na Jaji Dkt. Benhajj Masoud, mahakama ilipitia hoja tatu za msingi ambazo ni: kama Mahakama Kuu ilikuwa na uwezo kusikiliza shauli hilo, kama mdai aliweza kuthibitisha madai yake ya kudharirishwa, na hoja ya mwisho ni, kama mahakama ilitumia utaratibu sahihi kutoa nafuu amabazo zilitolewa na Mahakama Kuu.

Majaji hao watatu wa Mahakama ya Rufani walikubaliana na hoja za wakili wa utetezi wa mjibu maombi, Wakili Aliko Harry Mwamanenge na kuona kwamba hakika mahakama kuu ilikuwa na uwezo wakusikiliza kesi hiyo, nakwamba mjibu rufani alifanikiwa kuthibitisha madai yake ya kudharirishwa, na pia mahakama kuu ilitumia utaratibu sahihi kufikia tuzo ambayo ilitoa.

Hivyo mahakama ya Rufani haikuona sababu ya kubatilisha au kubadilisha chochote kwenye maamuzi ya mahakama kuu, na kuyabariki maamuzi hayo kama yalivyo.

Katika Kesi ya Msingi, Mahakama Kuu ilitoa uamuzi wa Gazeti la The Citizen kumlipa aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), ambaye kwa sasa ni Msajili wa Hazina Nehemia Kyando Mchechu, fidia ya shilingi Bilioni 2.5 baada ya kuthibitika kuwa, taarifa iliyochapishwa na gazeti hilo Machi 23, 2018 katika ukurasa wake wa mbele iliyokua na kichwa cha Habari ‘Kwa nini JPM alivunja Bodi ya NHC na kumng’oa Mchechu? haikuwa na ukweli wowote.