Home BUSINESS BENKI KUU: WATALII KURUHUSIWA KULIPA KWA FEDHA ZA KIGENI

BENKI KUU: WATALII KURUHUSIWA KULIPA KWA FEDHA ZA KIGENI

Thank you for reading this post, don't forget to subscribe!

ARUSHA

Benki Kuu ya Tanzania imetoa ufafanuzi kuhusu Kanuni za Matumizi ya Fedha za Kigeni za Mwaka 2025, ikieleza kuwa malipo ya bidhaa na huduma kati ya wakaazi na wageni, wakiwemo watalii, yanaweza kufanyika kwa kutumia fedha za kigeni.

Akizungumza katika mjadala uliofanyika kwenye Maonesho ya Karibu-Kilifair jijini Arusha tarehe 8 Juni 2025, Mkurugenzi wa Masoko ya Fedha wa Benki Kuu ya Tanzania, Bw. Emmanuel Akaro, alifafanua kuwa hatua hiyo inalenga kuwezesha mazingira rafiki ya kibiashara kwa wageni na urahisi wa miamala katika sekta ya utalii.

“Mawakala wa utalii ambao ni wakaazi, wanaruhusiwa kutumia fedha za kigeni kulipia huduma mbalimbali zinazotolewa kwa watalii kutoka nje ya nchi,”alisema.

Alisisitiza kuwa malipo yote kati ya wakaazi lazima yafanyike kwa Shilingi ya Tanzania, na ni kosa kwa mtoa huduma yeyote kukataa malipo yanayofanyika kwa kutumia Shilingi ya Tanzania.

Bw. Akaro aliongeza kuwa Kanuni hizi zimetungwa kwa mujibu wa Kifungu cha 26 cha Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania ya mwaka 2006, na zimeanza kutumika rasmi kuanzia tarehe 28 Machi 2025.

“Tangu kuanza kutumika kwa kanuni hizo, kumekuwa na matokeo chanya ikiwemo kuongezeka kwa ukwasi wa fedha za kigeni. Kwa mfano, miamala ya Dola za Marekani kwenye soko la fedha za kigeni la rejareja nchini imeongezeka kutoka wastani wa dola milioni 40 hadi milioni 69 kwa siku”, alisema.