Home LOCAL TAARIFA BINAFSI INA JUKUMU LA KULINDA HESHIMA NA HAKI ZA WATU –...

TAARIFA BINAFSI INA JUKUMU LA KULINDA HESHIMA NA HAKI ZA WATU – WAZIRI NAPE

Na: Mwandishi wetu Dodoma

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Mosses Nnauye amewataka watumishi wa Tume Ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi nchini (PDPC) kufanya kazi kwa ufanisi na kulinda imani Ya Tume hiyo na kuwaasa kutekeleza Sheria ya Tume bila kuwakera Wateja wao.

Waziri Nape amesema hayo Leo wakati akizindua Bodi ya Tume Ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi nchini (PDPC)) katika Ukumbi wa Mikutano wa TCRA jijini Dodoma.

Katika hatua nyingine Waziri Nape ameongeza kuwa Rais Dk.Samia Suluhu Hassan na Watanzania kiujumla wanaimani na Tume hiyo pamoja na Viongozi wake walioteuliwa Balozi Adadi Mohammed Rajabu kuwa mwenyekiti na Bi. Fatma Mohammed Ali kuwa kaimu huku akiwataka Viongozi hao kutengeneza Mpango mkakati ili Tume hiyo itoe Huduma za Viwango vya Juu na huduma hizo zitolewe katika Mfumo wa Kidigitali.

“Mnafahamu kuwa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilipitisha Sheria Na.11 ya mwaka 2022 ambayo ilianza kutekelezwa tarehe 01 Mei, 2023 hivyo msingi wa majukumu ya Bodi ni kuhakikisha Sheria na kanuni zinatekelezwa kwa ukamilifu lakini bila kuwa kikwazo kwa wateja wa Tume,”amesema Nape.

Pia amewataka Viongozi wa Tume hiyo kutekeleza majukumu yao kwani Tume hiyo ni Tume nyeti katika ukuaji wa Sayansi na Teknolojia akiongeza kuwa jambo hilo litafanya watu kutoka mataifa mbalimbali Duniani wakimbilie nchini kwani Tanzania ni nchi Salama.

“Kujitanganza na kutoa elimu kwa umma kuhusu uwepo na majukumu ya Tume kwani kwa sasa bado watu hawafahamu uwepo wa Tume hii hivyo mjipange vyema kusimamia suala hili na kuandaa makongamano ya kikanda na kimataifa ili kuwezesha upatikanaji wa fursa mbalimbali pamoja na wawekezaji ,“ amesema.

Aidha amesema kuwa Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi ina jukumu kubwa la kulinda heshima na haki za watu kwa kuhakikisha taarifa zao binafsi zinatumika kwa njia inayo zingatia haki, heshima,na utu wa mtu.

Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tume hiyo, Emmanuel Mkilia amesema kuwa Malengo ya Tume hiyo yamefikia asilimia 90 katika siku 100 toka Tume hiyo ianze kazi.

Amesema kuwa Malengo ya Tume hiyo ni Kutengeneza Utambulisho wa Tume kwa kutengeneza machapisho ya Wizara na kujenga jengo la Tume pia akaiomba Serikali kuongeza Wafanyakazi katika Tume kwani mpaka sasa Tume inawafanyakazi 16 pekee.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mohammed KHamis Abdulah amewapongeza watumishi wa Tume kwa kusema kuwa wamefanya juhudi kubwa mpaka kufikia kuzinduliwa kwa Tume hiyo haikua rahisi kukamilika katika kipindi cha siku 100 na wahakikishe watekeleza majukumu yake kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Miongozo mbalimbali ya kikanda na kimataifa.

Tume hiyo iliundwa mnamo tarehe 1 mwezi wa 5 mwaka 2023 ikiwa na jumla ya Watumishi 12 pekee.

Previous articleSOMA MAGAZETI YA LEO IJUMAA JANUARI 19-2024
Next articleKOCHA TAIFA STARS ASIMAMISHWA
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here