Home LOCAL JAJI MKUU AHIMIZA UTEKELEZAJI WA RIPOTI YA TUME YA HAKI JINAI

JAJI MKUU AHIMIZA UTEKELEZAJI WA RIPOTI YA TUME YA HAKI JINAI

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (kushoto juu) akimkabidhi vitendea kazi ‘instruments’ mmoja wa Hakimu Mkazi mpya alieapishwa katika hafla ya uapisho ulifanyika tarehe 10 Agosti, 2023 Mahakama Kuu, jijini Dar es salaam.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati waliosimama mstari wa juu) akishudia Hakimu Mkazi mpya akila kiapo katika hafla hiyo ya uapisho, Wengine ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Kuu na Kaimu Jaji Kiongozi, Mhe. Latifa Mansoor (kushoto mstari wa juu) na Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi (wa kwanza kulia mstari wa juu).

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati walioketi) akitoa hotuba mara baada ya kuwaapisha Mahakimu Wakazi 38 Wapya (hawapo pichani) katika hafla iliyofanyika Mahakama Kuu jijini Dar es salaam, Wengine ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Kuu na Kaimu Jaji Kiongozi, Mhe. Latifa Mansoor (kushoto) na Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi (kulia)

Sehemu ya Mahakimu Wakazi wapya 38 walioapishwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (hayupo pichana) wakifurahi jambo kwa kupiga makofi wakati wa hotuba fupi iliyotolewa na Jaji Mkuu mara baada ya uapisho huo.

(Picha na Innocent. Kansha- Mahakama)

Na: Magreth Kinabo- Mahakama

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma  amewataka Majaji, Mahakimu na Watendaji  wa Mahakama ya Tanzania kuanza kutekeleza ripoti ya mapendekezo ya  Tume ya Haki Jinai yanayohusu Mahakama ambayo hayahitaji fedha wala vikao.

Akizungumza katika halfa fupi ya uapisho wa  Mahakimu Wakazi 38 wapya jana tarehe 10 Agosti, 2023  Mahakimu Wakazi 38 wapya iliyofanyika katika Mahakama Kuu  Tanzania jijini Dar es Salaam, Mhe. Prof. Juma amesema baada ya taarifa ya Tume  hiyo kupokelewa na  Rais wa Jamhuri ya Muungano  wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mahakama iliunda Kamati ndogo kwa ajili ya kuipitia na kuchambua. 

Amesema Kamati hiyo, iliyoongozwa na Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Dkt. Gerald Ndika ilipitia ripoti hiyo na kuainisha maeneo yanayohusu Mahakama na kutoa ushauri wa namna bora ya kuyatekeleza na kuyafanyia ufumbuzi.

“Kamati ya Mahakama ilitambua maeneo 18 katika taarifa ya Tume ya Rais, ambayo yanayoihusu Mahakama moja kwa moja, yapo maeneo ambayo yanatekelezeka mara moja. Kuna mambo mengine hayasubiri fedha wala vikao, tunatakiwa kuanza kuyatekeleza inatubidi tuanze kubadilika na kufanyia maboresho,” amesema Jaji Mkuu.

Mhe. Prof. Juma ameongeza kuwa wakati ukifika atawaomba watendaji hao, kuanza kuyasoma maeneo hayo yote 18.

Alitaja eneo linalotakiwa kuanza kutekelezwa kuwa ni la adhabu, ambapo Tume ya Rais ilipendekeza Sheria irekebishwe ili kuipa Mahakama mamlaka ya kuzingatia muda mshtakiwa aliokaa mahabusu kama kigezo cha kupunguza muda wa adhabu ya kifungo.

“Kamati ya Mahakama ilisema (i)Kifungu cha 172 (2) (c) cha Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai, Sura ya 20 kinaitaka Mahakama inapotoa adhabu izingatie muda ambao mshtakiwa alikuwa mahabusu akisubiri usikilizwaji wa shauri bila kujali kama kosa linaangukia katika ukomo wa chini wa adhabu (minimum sentence),” amesisitiza.

Aidha, Jaji Mkuu amefafanua kwamba Kamati ya Mahakama imeshauri Mahakama zizingatie kifungu tajwa hapo juu pamoja na sheria nyingine zinazoipa Mahakama utashi wa kutoa adhabu nafuu.

Kamati ya Mahakama ilikumbusha kuwa, tayari Mahakama inao Mwongozo wa Mahakama wa Utoaji Adhabu (Sentencing Guidelines, 2023, hivyo Mahakimu na Majaji wautumie huu muongozo.  Huku akisisitiza kwamba suala hilo litafuatiliwa kwa takwimu ili kuona linatekelezwa.

Jaji Mkuu Mhe. Prof. Juma amebainisha kuwa Tume ya Rais iliona changamoto ya matumizi hafifu ya adhabu mbadala.

“Kamati ya Mahakama imesema Maafisa wa Mahakama waendelee kukumbushwa kutoa adhabu mbadala kama ilivyoainishwa katika waraka wa Jaji Kiongozi Na. 5 wa mwaka 2005 unaosisitiza kutolewa kwa adhabu mbadala ili kupunguza msongamano magerezani,” amesema.  

Hivyo amewakumbusha Majaji na Mahakimu kutumia adhabu mbadala kulingana na sheria, taratibu na viapo vyao na kuacha kukimbilia vifungo ambavyo vinachangia kuwepo kwa msongamano wa wafungwa magerezani.

Awali tarehe 15 Julai, 2023 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan  alipokea ripoti ya tume hiyo na alizitaka Taasisi za Haki Jinai kufanya marekebisho ambayo hayana gharama za kifedha katika mifumo yao ya kiutendaji ili kuleta haki kwa wananchi. 

Tume ya  hiyo ilikuwa na kazi ya kukusanya maoni kutoka taasisi 12 kwa lengo la kupata ushauri na mapendekezo ya namna bora ya kuimarisha mfumo na utendaji kazi wa taasisi zinazohusika na haki jinai. 

Januari mwaka huu, Rais Samia aliunda Tume hiyo yenye wajumbe 11 wakiongozwa na Mwenyekiti, Jaji Mkuu mstaafu, Mohamed Othman Chande huku Katibu wa Tume hiyo akiwa ni Balozi Omeni Sefue ambaye ni Katibu Mkuu Kiongozi mstaafu.

Previous articleRAIS DKT. SAMIA AIPONGEZA BENKI YA NMB KWA MCHANGO WAKE KATIKA. KILIMO
Next articleWIZARA YA MALIASILI NA UTALII YAPONGEZWA KWA KUPAMBANA NA CHANGAMOTO YA MIGONGANO BAINA YA BINADAMU NA WANYAMAPORI
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here