Waziri katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Prof. Joyce Ndalichako akisalimiana na baadhi ya wafanyakazi wa kampuni ya GGML alipotembelea banda la kampuni hiyo kwenye maonesho ya afya na usalama mahali pa kazi yaliyofikia tamati tarehe 30 Aprili 2023.
Mfanyakazi wa Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML), Omary Faustine Matulanya akitoa maelezo kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Patrobas Katambi (kushoto) kuhusu matairi yanayotumika kwenye mitambo ya ubebaji mawe na mchanga wa dhahabu kutoka ndani ya migodi. Katambi alitembelea banda la kampuni hiyo kwenye maoneosho ya afya na usalama mahali pa kazi yaliyofanyika kwenye viwanja vya Tumbaku mkoani Morogoro kuanzia tarehe 26 hadi 30 Aprili mwaka huu
Na: Mwandishi Wetu
NAIBU Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na watu wenye Ulemavu, Patrobas Katambi ameipongeza Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) kwa kutoa fursa za ajira kwa Watanzania zaidi ya asilimia 90 ndani ya mgodi huo pamoja na kuwapatia wazawa fursa za kutoa huduma za kuuza bidhaa za ndani kwenye kampuni hiyo.
Pia ameipongeza kwa kuibuka mshindi wa ubunifu na banda bora kwenye maonesho ya afya na usalama mahali pa kazi yaliyofanyika katika viwanja vya Tumbaku mkoani Morogoro kuanzia tarehe 26 hadi 30 Aprili mwaka huu.
Katambi ametoa pongezi hizo mwishoni mwa wiki alipotembelea banda la kampuni hiyo katika maonesho hayo yaliyoratibiwa na Wakala wa Afya na Usalama mahali pa kazi (OSHA).
“Niwapongeze hasa kwa kupunguza ulemavu kazini, magonjwa yanayotokana na kazi lakini pia kuhakikisha kwamba mazingira yote ya kufanyia kazi yanakuwa salama.
“Nafurahi kuona kwamba banda zima na hata ndani ya kampuni asilimia kubwa ya wafanyakazi ni watanzania wenzetu kwa maana hiyo tunazidi kusisitiza kwamba kwenye maeneo yote ya kazi watanzania ni kipaumbele,” amesema.
Amesema mgeni anaposhika nafasi ya ajira ina maana kwamba ujuzi huo ni adimu, mtanzania hana sifa wala vigezo lakini pamoja na hilo Rais Samia Suluhu Hassan ameelekeza watanzania wajengewe uwezo kushika nafasi hizo.
“Ameelekeza kuhakikisha wakati wote kwamba wakiwepo wageni wenye ujuzi nyuma yake awepo mtanzania anayejifunza hizo kazi na baada ya muda, utaalamu tubaki nao wenyewe,” amesema.
Ameongeza GGML imekuwa mfano wa kuigwa katika manunuzi yanayofanyika kwenye migodi yake kwa sababu Serikali kupitia mpango wa kuwezesha wazawa kutoa huduma na kuuza bidhaa ndani ya mgodi (local content) inasisitiza kwamba vitu kama vipo hapa nchini vinunuliwe hapahapa ili kiuongeza ukwasi ndani ya nchi ili fedha nyingi isitoke nje.
“Pia mmezingatia usalama wa mazingira kwa ujumla ili tusipate watu wenye ulemavu unaotokana na migodi hata pia mazingira na ardhi yetu inabaki kuwa salama kwa hiyo nyinyi watanzania mliopo huko ni wawakilishi wa kuhakikisha usalama unakuwepo…wa kwetu sisi, viumbe hai,” amesema.
Aidha, akimkaribisha katika banda hilo, Meneja anayehusika na usalama kazini kutoka GGML, Isack Senya amesema zaidi ya wananchi 3000 wametembelea banda hilo na kujifunza mambo mbalimbali kuhusu teknolojia zinazotumika kufanya kazi katika mazingira yenye afya na usalama.
Amesema mwaka huu GGML ilileta vifaa vya kiteknolojia na kisasa kiasi cha kuiwezesha kampuni hiyo kuibuka kampuni bora yenye ubunifu kwenye vifaa hivyo.
Pia amemuahidi Naibu Waziri kuendelea kutekeleza miradi mbalimbali inayosaidia jamii kuondokana na umaskini pamoja na kupata huduma bora kwa kushirikiana na serikali.
Pamoja na mambo mengine, Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na watu wenye Ulemavu, Prof. Joyce Ndalichako naye alipita katika banda hilo na kuipongeza kampuni hiyo kwa kuwa mdau muhimu katika kuzingatia matakwa ya sheria yanayosisitiza afya na usalama mahali pa kazi.