Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa kumekuwa na tabia ya baadhi ya watu
kuwatumikisha watoto katika maeneo ya machimbo ya madini na kuwanyima fursa watoto hao wa Kitanzania kupata haki yao ya msingi ya elimu.
Ametoa agizo hilo leo (Jumatatu, Februari 13, 2023) wakati akizungumza na wananchi baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa hospitali ya wilaya ya Songwe inayojengwa katika kata ya Mkwajuni akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Songwe.
Waziri Mkuu amesema viongozi wa machimbo ya madini katika maeneo mbalimbali nchini wafanye uhakiki wa watu wote wanaofanya kazi katika maeneo hayo na wahakikishe watoto wote walio kwenye umri wa kwenda shule wanapelekwa.
“Kumeibuka tatizo la ukatili wa kuwatumikisha na vitendo vya hovyo wanavyofanyiwa watoto wetu kwenye maeneo hayo fanyeni uchungu na kubaini wanaohusika na vitendo hivyo. Mkuu wa wilaya hakikisha unatokomeza ukatili kwa watoto na wanawake.”
“Viongozi katika mikoa yote nchini wachukulieni hatua wazazi wanaoshindwa kuwasimamia watoto wao kwenda shule. Wananchi shirikianeni kuhakikisha watoto wenye umri wa kwenda shule wanakwena shule, mtoto wa mwenzio ni wako.”
Pia, Waziri Mkuu amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Songwe, Cecilia Kavishe ahakikishe ujenzi wa mradi wa hospitali hiyo ukamilika katika kipindi cha mwezi mmoja na nusu na ifikapo Aprili ianze kutoa huduma.
“Katika kipindi cha miaka miwili ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan hakuna mahali ambapo hapajaguswa na miradi ya maendeleo, kamilisheni ujenzi wa majengo haya ili wananchi wapate huduma karibu na makazi yao.”
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Songwe, Cecilia amesema mradi wa ujenzi wa hospitali ya wilaya hiyo hiyo ambao umefikia asilimia 95 umegharimu shilingi bilioni 3.5 na unatarajiwa kukamilika Machi 31, 2023.
Amesema ujenzi wa hospitali hiyo unahusisha majengo ya huduma za wagonjwa wa nje, mionzi, maabara, wodi tatu za magonjwa mchanganyiko, famasia, utawala, mama na mtoto, huduma ya dharura, upasuaji, uchunguzi, jengo la kuhifadhia maiti na wodi mbili za upasuaji.
Naye, Mbunge wa jimbo la Songwe, Philipo Mulugo ametumia fursa hiyo kumshukuru Rais Dkt. Samia kwa kuridhia utoaji wa fedha ambazo zinatumika katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo jimboni humo ikiwemo ya afya, maji na elimu.
Hata hivyo mbunge huyo ameiomba Serikali iwajengee kwa kiwango cha lami barabara ya kutoka Mbalizi-Changombe-Mkwajuni-Saza-Patamela-Makongorosi yenye urefu wa kilomita 118 ili kurahisisha usafiri wa watu na mizigo.