Na. WAF – Dodoma
Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Seif Shekalaghe leo amekabidhiwa rasmi ofisi na aliyekuwa Katibu Mkuu Prof. Abel Makubi mara baada ya kuapishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Makabidhiano hayo yamefanyika katika Ofisi za Wizara ya Afya zilizopo Mji wa Serikali, Mtumba Jijini Dodoma.
Makabidhiano hayo yamehudhuriwa na Viongozi mbalimbali na watumishi wa Wizara hiyo.
Akiongea mara baada ya makabidhiano hayo Katibu Mkuu Dkt. Shekalaghe ameahidi utumishi ulio bora na kwamba ataendelea kutekeleza kazi na majukumu yote ambayo yamekuwa yakiendelea katika sekta ya afya nchini pamoja na kutoa ushirikiano wa kutosha katika kuboresha upatikanaji wa huduma bora za afya.
Aidha, amemshukuru Prof. Makubi kwa kuonesha ukomavu wa uongozi pia kumuelekeza baadhi ya mambo ambayo hakuyajua.
“Nakushukuru sana nimejua mengi kutoka kwako kwakuwa tumefanya kazi pamoja kwa muda wa mwaka mmoja nikiwa Naibu Katibu Mkuu na wewe ukiwa Katibu Mkuu,” amesema Dkt. Shekalaghe.
Dkt. Shekalaghe amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kumuamini na kumteua katika nafasi hiyo.