Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akisalimiana na Katibu Mkuu wa Kanisa la Africa Inland Church Tanzania (AICT) Mchungaji Josephales Mtebe pamoja na Katibu wa Jumuiya ya kikristo Tanzania Mchungaji Moses Matonya mara baada ya kuwasili katika Kanisa la AICT Magomeni Jijini Dar es salaam katika Ibada ya Kusimikwa Askofu wa AICT Dayosisi ya Pwani Askofu Philipo Mafuja Magwano leo tarehe 29 Januari 2023. Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akiwa na Mkewe Mama Mbonimpaye Mpango wakishiriki Ibada ya Kusimikwa Askofu wa Kanisa la Africa Inland Church Tanzania (AICT) Dayosisi ya Pwani Askofu Philipo Mafuja Magwano iliofanyika katika Kanisa la AICT Magomeni Jijini Dar es salaam leo tarehe 29 Januari 2023.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akimpongeza Askofu wa Kanisa la Africa Inland Church Tanzania (AICT) Dayosisi ya Pwani Askofu Philipo Mafuja Magwano pamoja na mkewe Elizabeth Manumbu mara baada ya Kusimikwa katika Ibada iliofanyika katika Kanisa la AICT Magomeni Jijini Dar es salaam leo tarehe 29 Januari 2023.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akizungumza na waumini wa kanisa la Kanisa la Africa Inland Church Tanzania (AICT) mara baada ya Ibada ya Kusimikwa Askofu wa Kanisa la Africa Inland Church Tanzania (AICT) Dayosisi ya Pwani Askofu Philipo Mafuja Magwano iliofanyika katika Kanisa la AICT Magomeni Jijini Dar es salaam leo tarehe 29 Januari 2023.
PICHA – OFISI YA MAKAMU WA RAIS
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango pamoja na Mkewe Mama Mbonimpaye Mpango leo tarehe 29 Januari 2023 wameungana na waumini wa Kanisa la Africa Inland Church Tanzania (AICT) katika Ibada ya Kusimikwa Askofu wa AICT Dayosisi ya Pwani Askofu Philipo Mafuja Magwano iliofanyika katika Kanisa la AICT Magomeni Jijini Dar es salaam.
Ibada hiyo imeongozwa na Askofu Mkuu wa Kanisa hilo Mussa Masanja Magwesela na kuhudhuriwa na Maaskofu wa Dayosisi mbalimbali wa Kanisa hilo, viongozi wa Serikali, pamoja na viongozi wa dini kutoka madhehebu mengine.
Akizungumza mara baada ya kumalizika kwa Ibada hiyo, Makamu wa Rais amewasihi viongozi wa dini kuifanya kazi ya kumtumikia Mungu kwa uaminifu, uthabiti, uhodari na kwa moyo wa upendo kutokana na kazi hiyo kuwa ya heshima sana. Amesema jamii ina imani na matarajio makubwa kutoka kwa viongozi wa dini. Makamu wa Rais ameongeza kwamba katika ulimwengu wa sasa limezuka wimbi la baadhi ya viongozi wa dini kuenenda isivyostahili wito wao ikiwemo baadhi yao kuwa na tamaa ya kujilimbikizia mali isivyo halali au uchu wa madaraka na hivyo kusababisha mafarakano ndani ya nyumba za ibada.
Makamu wa Rais ametoa wito kwa Viongozi wa Dini hapa nchini kuongeza nguvu zaidi katika kulea taifa kimaadili na kukemea maovu. Amewaasa kuendelea kuisaidia Serikali kukemea vitendo ambavyo ni chukizo kwa Mungu na vinaenda kinyume na maadili ya kitanzania kama vile, ubakaji, ulawiti, ushoga, ukahaba, matumizi ya madawa ya kulevya, rushwa na ukatili dhidi ya wanawake na Watoto,ndoa na mimba za utotoni na matumizi ya mavazi yasiyo na staha.
Makamu wa Rais ameongeza kwamba kuporomoka kwa maadili ni jambo lenye athari mbaya kwa jamii na Taifa kwa ujumla na kunachangia kwa kiasi kikubwa kurudisha nyuma juhudi za kuharakisha maendeleo ya Tanzania.
Aidha Makamu wa Rais amewasihi viongozi wa dini zote kuendelea kuliombea taifa amani na kuwahimiza waumini hususani vijana kufanya kazi kwa bidii ili kujiletea maendeleo. Pia amewaomba viongozi wa dini kuendeleza ushirikiano uliopo kupitia Kamati za Amani na Jumuiya ya Maridhiano Tanzania. Amesema serikali iko tayari na inaahidi kushirikiana na viongozi wa madhehebu yote kuhakikisha watanzania wanaishi kwa amani katika nchi yao.
Makamu wa Rais amewaasa viongozi wa dini kutilia mkazo usafi na utunzaji wa mazingira. Amesema kutokana na nafasi waliopewa na Mwenyezi Mungu, Viongozi wa dini wanaweza kupaza sauti na kuhamasisha usafi na utunzaji wa mazingira majumbani na maeneo ya Ibada. Amewaomba kuendelea kukemea ukataji hovyo wa misitu na kuhamasisha upandaji wa miti nchini kote hususan katika msimu huu wa mvua zinazoendelea kunyesha.
Makamu wa Rais amesema Serikali itaendeleza uhusiano uliopo baina yake na madhehebu ya dini ikiwa ni pamoja na kuhakikisha madhehebu ya dini yanaendelea kutekeleza wajibu wake kwa uhuru na kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania toleo la 1977. Ameongeza kwamba tayari
Serikali inazifanyia kazi changamoto za Kanisa la African Inland Church Tanzania ikiwemo za umiliki wa Kiwanja Na. 66B kilichopo barabara ya Makongoro, Mwanza na pia Shule za Sekondari za Kahunda (Buchosa) na Buhima (Busega).
Awali akitoa Mahubiri wakati akiongoza Ibada hiyo Askofu Mkuu wa Kanisa la African Inland Church Tanzania (AICT) Mussa Magwesela amewaomba waumini kuendelea na wajibu muhimu wa wakristo wa kuwatia moyo viongozi wa dini, kuwasikiliza , kuwaombea, kuwasaidia mahitaji yao pamoja na kuwakaribisha katika familia.
Akitoa salamu za shukrani mara baada ya kusimikwa kuwa Askofu wa Kanisa la African Inland Church Tanzania (AICT) Dayosisi ya Pwani Askofu Philipo Mafuja Magwano amewaomba viongozi wa dini kushirikiana katika kufundisha kwa usahihi neno la Mungu na sio jambo lingine ili kuweza kuisaidia serikali katika kupambana na wahalifu na waovu katika taifa.
Askofu Mwagwano amesema ataendelea kushirikiana na Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kujenga ustawi wa taifa. Aidha ametoa rai kwa wazazi hapa nchini kuhakikisha wanaona umuhimu wa elimu kwa kuwapeleka watoto shuleni kupata elimu ambayo ni ufunguo wa Maisha.