Home Uncategorized TUMIA NISHATI JADIDIFU, PUNGUZA GHARAMA ZA UMEME

TUMIA NISHATI JADIDIFU, PUNGUZA GHARAMA ZA UMEME

*Mabadiliko ya tabia nchi ni vita ya dunia

Na: Jimmy Kiango

DUNIA sasa inayatazama athari za mabadiliko ya tabia nchi kama vita ambavyo vinapaswa kupiganwa na mataifa yote duniani.

Katika kufanikisha mwelekeo huo serikali ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania na yenyewe sasa ipo katika maandalizi ya kuandaa Mkakati wa Kitaifa wa Nishati Jadidifu ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Nia hiyo ya serikali imebainishwa  hivi karibuni jijini Dar es Salaam na Mkuu wa Kitengo cha Usimamizi wa Mazingira kutoka Wizara ya Nishati, Emilian Nyanda, katika warsha ya kuwajengea uwezo waandishi wa habari iliyoandaliwa na Taasisi ya Kuendeleza Nishati Endelevu na Uhifadhi wa Mazingira Tanzania(TaTEDO).

Nyanda alisema  serikali imeandaa Mkakati wa Kitaifa wa Nishati Jadidifu kupitia Wizara ya Nishati ili kuongeza mchango wa Nishati Jadidifu katika upatikanaji wa nishati ya umeme nchini.

Nishati Jadidifu ni vyanzo vya kuzalisha umeme  visivyoisha ikiwemo  upepo, jua, joto ardhi, mawimbi ya bahari, maporomoko ya maji ambayo ni chini ya megawati 10 na vinginevyo ambavyo vina uwezo wa kuzalisha nishati bila kuchafua mazingira.

“Kupitia Sera yake ya Taifa ya Nishati ya mwaka 2015 serikali inaweka kipaumbele katika uendelezaji wa rasilimali za nishati jadidifu kwa kuwa ni rasilimali endelevu na nyingi zinapatikana hapa nchini.

“Katika sekta ya Nishati ukitaka upunguze athari za mabadiliko ya tabia nchi ni lazima utumie nishati jadidifu na matumizi bora ya nishati.

“Sera yetu inatambua nishati jadidifu lakini na sera zingine kama ya Mazingira ya Mwaka 2021 na Mkakati wa Kitaifa wa Mazingira ambazo zote hizo ni muendelezo wa nishati jadidifu,” alisema Nyanda.

Aliweka wazi kuwa  kuwa kukamilika kwa mkakati huo kutatoa muongozo mzuri wa uendelezaji wa nishati jadidifu hapa nchini.

“Mpango wa sasa wa wizara nikuandaa mkakati wa kitaifa wa Nishati Jadidifu na tupo katika hatua nzuri na tayari mshauri elekezi ameshaanza maandalizi ya mkakati na kwa sasa anaendelea kupata maoni ya wadau hadi mwakani mwezi wa pili itakuwa imekamilika.

“Hivyo wanahabari mnao wajibu wa kutusaidia kutoa elimu ya umuhimu wa hii rasilimali ya Nishati Jadidifu ili wananchi wetu wajue jinsi serikali yao ilivyojipanga kuendeleza nishati hizo,” amesema Nyanda na kuongeza kuwa:

“Changamoto nyingine iliyokuwepo ni Sera ya Mkakati wa Nishati Jadidifu na jinsi gani unapata nyenzo ya kutekeleza sera yako inayotambua nishati Jadidifu ndio maana sasa hivi serikali imewekeza katika kuandaa Mkakati ya Nishati Jadidifu na Mkakati wa Matumizi Bora ya Nishati,” amesema Nyanda.

Hata hivyo Nyanda ameongeza kuwa mbali na mkakati huo  pia wanaandaa mkakati wa matumizi bora  ya nishati ili viende pamoja na sera ya mkakati wa nishati jadidifu.

Kwa upande wake Mratibu wa Mabadiliko ya Tabianchi  na Tungamotaka kutoka TaTEDO, Shima Sago amesema wanazungumzia Nishati Jadidifu hasa wakati huu kutokana na kwamba nishati zingine zinachangia uharibifu wa tabaka la juu linazozuia mionzi ya jua kufika ardhini hivyo kusababisha ongezeko la joto na ukame.

“Faida za Nishati Jadidifu ni pamoja na kupunguza gharama za kununua umeme mara kwa mara,kutoa ajira,kukaushia vyakula shambani,kuepuka matatizo ya kiafya kwa kuvuta hewa chafu,kupunguza hewa ukaa na kutunza tabaka la kuzuia mionzi ya jua.

“Ili upate tani moja ya mkaa lazima ukate magogo 12 ya miti na kwa mwaka tunatumia tani Milioni 2.5 za mkaa nchini hivyo ni lazima tuendeleze kuhifadhi mazingira na kutumia nishati jadidifu kwa ajili ya vizazi vya sasa na vijavyo”amesema Sago.

Previous articleMAENEO ZAIDI YAANDALIWE KWA UZALISHAJI WA NISHATI JADIDIFU
Next articleUZINDUZI WA BARABARA BABATI MJINI PAMOJA MAGHALA YA KUHIFADHIA CHAKULA MKOANI MANYARA
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here