Home BUSINESS KITS KULETA MAWAKALA WA UTALII ZAIDI 30 KUTOKA NCHINI MAREKANI.

KITS KULETA MAWAKALA WA UTALII ZAIDI 30 KUTOKA NCHINI MAREKANI.

Mkurugenzi wa Wellworth Hotel, Bw. Sameer Ismail (kushoto), akizungumza na waandishi wa habari kuhusu ujio wa ugeni wa mawakala wa utalii zaidi 30 kutoka nchini Marekani.

Kaimu Mkurugenzi wa Masoko wa Bodi ya Utalii Nchini (TTB) Felix John (kushoto) akiwa na Afisa Uendeshaji Mkuu wa Kampuni ya Kimataifa inayojihusisha na masuala ya Utalii ya Kilimanjaro International Tourism & Safaris (KITS), Bw. Francis Malugu, akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam kuhusu ujio wa ugeni wa Mawakala wa Utalii zaidi ya 30 kutoka nchini Marekani.

Afisa Uendeshaji Mkuu wa Kampuni ya Kimataifa inayojihusisha na masuala ya Utalii ya Kilimanjaro International Tourism & Safaris (KITS), Bw. Francis Malugu akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam kuhusu ujio wa ugeni wa Mawakala wa Utalii zaidi ya 30 kutoka nchini Marekani.

Ripoti ya: Noel Rukanuga, Fullshangwe Blog, DAR ES SALAAM.

KAMPUNI ya kimataifa inayojihusisha na masuala ya utalii ya Kilimanjaro International Tourism & Safaris (KITS), inatarajia kupokea ugeni wa Mawakala wa Utalii zaidi ya 30 kutoka nchini Marekani, Ufaransa na Lithuania kuanzia Novemba 23, mwaka kwa ajili ya kuwawakilisha maelfu ya watalii kutoka nchi mbalimbali duania ambao wanatarajiwa kutemebelea Tanzania.

Kampuni ya KITS imekuwa balozi mzuri na kuwa lango la kuingiza watalii na wawekezaji kutoka majimbo yote 50 ya nchini Marekani.

Inaelezwa kuwa mafanikio ya ujio wa mawakala hao umechangiwa kwa kiasi kikubwa na hatua ilizochukua KITS baada ya kuona taarifa za Rais Samia Suluhu Hassan akishiriki kutengeneza makala ya filamu ya kutangaza vivutio vya utalii duniani ijulikanayo kama “Royal Tour” ambayo kwa awamu hii imefanyika nchini Tanzania.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Afisa Uendeshaji Mkuu wa Kampuni ya KITS Bw. Francis Malugu, amesema kuwa kazi ya kuwataarifu Mawakala hao wa utalii kuhusu filamu hiyo ya ‘Royal Tour’ ilifanywa na kampuni hiyo ya KITS, yenye Makao Makuu yake jijini nchini Marekani na ofisi zake za uendeshaji zilizo jijini Arusha.

“Mara baada ya kupata taarifa mapema za utengenezaji wa makala hiyo ya filamu na kwamba Rais Samia Suluhu Hassan ndiye atakayekuwa muongozaji mkuu, tuliwataarifu mawakala wa Utalii katika vyama vya utalii duniani ambavyo KITS ni mwanachama wake na zaidi ya mawakala 30 waliomba na kuthibitisha kuja kuitembelea Tanzania, Novemba mwaka huu.” amesema Bw. Malugu.

Bw. Malugu amempongeza Rais Samia kwa uamuzi aliouita wa busara na wa makusudi wa kuitangaza Tanzania kupitia ziara hiyo maarufu ya “Royal Tour”.

Amesema kuwa itasaidia kuongeza nguvu katika utekelezaji wa mipango ya Serikali ya kukuza uwekezaji na kuvutia utalii kama ambavyo KITS imekuwa ikifanya nchini Marekani.

Bw.Francis Malugu amesema kuwa kukamilika kwa makala ya filamu itasaidia kurahisisha shughuli za utangazaji utalii ambazo kampuni ya KITS imekuwa ikizifanya katika nchi mbalimbali.

Bw. Malugu amebainisha kuwa wanatarajia kushiriki mikutano na matukio ya kimataifa itakayofanyika kuanzia Oktoba 10 hadi 11 mwaka huu nchini Ufaransa katika onesho la ‘Top Resa’, Travel Adventure Show majiji ya Atlanta, Georgia na San Francisco, California.

Amesema kuwa tukio jingine kubwa wanalokwenda kushiriki KITS ni pamoja na National Tour Association (NTA) Annual Convention linalofanyika jijini Clevelend, Ohio ambalo litahusisha mawakala wa utalii zaidi ya 2,300 kutoka majimbo yote ya Marekani na nchini Canada.

“Ni matarajio yetu kuwa kama makala hiyo itakuwa imekamilika katikati mwa Novemba, KITS itatumia ushawishi wake kueneza kwa wateja wake juu ya kuonyeshwa kwa makala hiyo ya Rais Samia wakati wa tukio la ufunguzi wa Kongamano hilo.” amesema Malugu.

Bw.Francis Malugu ametoa shukrani za dhati kwa ushirikiano ambao kampuni yao imekuwa ikipewa na mamlaka mbalimbali za serikali ukiwemo ubalozi wa Tanzania nchini Marekani, Bodi ya Utalii Tanzania, Mamlaka za Hifadhi za TANAPA, TAWA na Ngorongoro, Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na Kituo cha Mikutano cha kimataifa cha Arusha (AICC) taasisi ambazo zina dhamana ya kuendeleza utalii hapa nchini.

Ameeleza kuwa matarajio yao kuwa makala hii inayorekodiwa na Mhe.Rais Samia itakuwa nyenzo muhimu katika shughuli za utangazaji zinazoendelea ili kuisaidia nchi kufikia lengo la watalii millioni 5 na mapato ya dola za kimarekani bilioni 6 ifikapo mwaka 2025 licha ya kuwepo kwa changamoto za Uviko 19 zinayoikabili dunia.

Amesema kuwa itasaidia kuitambua Tanzania kama sehemu mahususi ya asili ya dunia ambayo kila mpenda utalii duniani anapaswa kuitembelea.

Bw. Malugu amesema wao kama wadau wa sekta ya utalii wameupa uzito uamuzi huo na wanampongeza kwa moyo wa dhati Mh.Rais Samia na kuunga mkono juhudi anazozichukua za kuimarisha sekta ya utalii ikiwa ni miongoni mwa sekta zenye mchango mkubwa hapa nchini.

Ametoa wito kwa serikali na balozi wa Tanzania nchini Marekani kama itampendeza, wakati Rais Samia akifika nchini Marekani kwa ajili ya uzinduzi wa filamu hiyo itakayoanza kuoneshwa Novemba mwaka huu, kutoa fursa ya kushiriki kwa watanzania wanaojihusisha na kushawishi watalii kuja nchini kutalii na kuwekeza.

Ameeleza kuwa lengo lao ni kuchangia ukuaji wa uchumi kutokana na kazi wanazozifanya za kuongoza watalii, kuvutia watalii, kutoa utalaamu wa ukuzaji wa biashara hasa ya utalii kwa kutangaza vivutio vya kitalii, kutoa elimu kwa taasisi na makundi mbalimbali pamoja na kuvutia uwekezaji.

”Ni faraja kwa serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan ambayo imekuwa ikihamasisha mabalozi na watanzania waishio nje ya nchi kutangaza vivutio vya utalii na uwekezaji” amesema Malugu.

Previous articleEQUITY BANK (T) NA PASS TRUST WAKUBALIANA DHAMANA ZA MIKOPO YA KILIMO ILI KUONGEZA NEEMA KWA WAKULIMA NCHINI
Next articleSAFARI YA MWISHO YA ZACHARIA HANS POPPE
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here