Home ENTERTAINMENTS UZINDUZI WA ALBAMU MBILI ZA MAMAJUSI ANGLIKANA MOSHI, ZAIDI YA MILIONI NANE...

UZINDUZI WA ALBAMU MBILI ZA MAMAJUSI ANGLIKANA MOSHI, ZAIDI YA MILIONI NANE ZAPATIKANA INJILI YAENEZWA

 Na: Maiko Luoga MOSHI.

Waimbaji wa nyimbo za Injili wametakiwa kutumia vipawa vyao walivyojaliwa na Mwenyezi Mungu kuwahubiria watu kuacha matendo mabaya na kuishi maisha ya kumpendeza Mungu na Jamii inayo wazunguka ili kuendeleza umoja na mshikamano wa Taifa.

Wito huo umetolewa Juni 13, 2021 na Mbunge wa Jimbo la Arumeru Mashariki Mkoani Arusha Dkt, John Pallangyo alipokuwa Mgeni rasmi kwenye uzinduzi wa albamu mbili za SIMAMA YESU UNITETEE na PAJI LA USO zilizoimbwa na Kwaya ya Mamajusi iliyopo chini ya Kanisa Anglikana Moshi Dayosisi ya Mount Kilimanjaro DMK.  

“Waimbaji mnatakiwa kutumia karama zenu mlizopewa na Mungu kutangaza injili ili watu waache dhambi, hii itasaidia kuendeleza Taifa letu lenye Amani, umoja na mshikamano, mimi ni mdau wa Kwaya hii ya Mamajusi tangu mlipoanza huduma ya uimbaji ndio maana leo nimekubali kuja kuwaunga mkono” alieleza Mhe, Dkt, John Pallangyo.

Titus Sambay Mwalimu wa Kwaya ya Mamajusi na Katibu wa Kwaya hiyo amesema pamoja na tukio la uzinduzi wa Albamu hizo mbili lililotanguliwa na Ibada, wamefanya harambee ya kupata fedha kwaajili ya kununua vyombo vipya vya muziki kwakuwa vinavyotumika sasa vimechakaa kutokana na kudumu kwa kipindi cha miaka mingi. 

Amesema katika harambee hiyo jumla ya fedha za Kitanzania kiasi cha milioni nane na laki sita zimepatikana, kati ya hizo Mbunge wa Arumeru Mashariki aliyekuwa Mgeni Rasmi ametoa kiasi cha shilingi milioni moja na fedha nyingine ni michango ya wadau walioshiriki tukio hilo.

Emmanul Mangare Mwenyekiti wa Kwaya ya Mamajusi ametumia nafasi hiyo kuwashukuru washiriki wa tukio hilo na kuahidi kuendelea kutangaza injili ya Kristo kwa njia ya uimbaji ili watanzania na Mataifa mengine wajue habari njema za Mwenyezi Mungu. 

Bw, Yohana Mdoe, Bi, Pendo Sambay na Bi, Hellen Kimaya wamesema mafanikio ya Kwaya ya Mamajusi yametokana na umoja walioudumisha kwa kipindi cha muda mrefu tangu mwaka 1975 Kwaya hiyo ilipoanzishwa ikiwa na waimbaji nane na sasa ina zaidi ya Waimbaji 85 wakiendelea kutangaza injili ndani na nje ya mipaka ya Tanzania.
Previous articleDIWANI WA LIWITI KUZINDUA WIKI YA KERO KESHO JUNI 13
Next articleMTENDAJI LIWITI, APIGA MARUFUKU MADALI,WENYUMBA KUPANGISHA LAZIMA WAPANGAJI WASAJILIWE DAFTARI LA MAKAZI.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here