Home BUSINESS WADAU ZAIDI YA 500 SEKTA BINAFSI NA UMMA KUJADILIANA KUBORESHA MAZINGIRA YA...

WADAU ZAIDI YA 500 SEKTA BINAFSI NA UMMA KUJADILIANA KUBORESHA MAZINGIRA YA BIASHARA NA UWEKEZAJI NCHINI

Naibu Katibu Mkuu WIZARA ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara Ally Gugu (katikati) akizungumza na waandishi wa habari (hawamo pichani) katika mkutano na waaandishi hao uliofanyika leo Februari 1, 2023 kwenye Ofisi za BRELA Jijini Dar es Salaam, kuhusu Mkutano wa Majadiliano kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi utakaofanyika Februari 2, 2023 katika ukumbi wa kimataifa wa mikutano wa Mwl. Julius Nyerere uliopo Jijini humo.

Katibu Mtendaji wa TNBC, Dkt. Godwill Wanga akijibu moja ya maswali yaliyoulizwa na waandishi wa habari, juu ya suala zima la uboreshaji mazingira ya Biashara Nchini Tanzania.

Naibu Katibu Mkuu WIZARA ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara Ally Gugu (kaulia) akimsikiliza Katibu Mtendaji wa TNBC, Dkt. Godwill Wanga (katikati) alipokuwa akijibu maswali yaliyoulizwa na wanahabari katika mkutano huo.

 

Mkurugenzi wa Bodi ya TPSF Bw. Octavian Mshiu akielezea  namna ambavyo Serikali ya Awamu ya sita ya Rais Samia Suluhu Hassan ilivyofanikiwa kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji na Biashara Nchini. (kushoto) ni, Naibu Katibu Mkuu WIZARA ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara Ally Gugu

Sehemu ya waandishi wa habari na wadau walioshiriki katika mkutano huo.

(PICHA NA: HUGHES DUGILO)

NA: HUGHES DUGILO, DSM

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara Ally Gugu amesema kuwa Wizara hiyo inaendelea na jitihada za kuimarisha mazingira ya kufanyia Biashara na uwekezaji nchini Tanzania kwa kuendeleza utekelezaji wa Mpango wa Kuimarisha Mazingira ya Biashara nchini (MKUMBI), na kuboresha upatikanaji wa huduma mbalimbali zikiwemo miundombinu.

Gugu ameyasema hayo katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika leo Februari 1,2023 kwenye Ofisi za BRELA Jijini Dar es Salaam kuhusu Mkutano wa Majadiliano kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi unaotarajiwa kufanyika Februari 2, 2023 katika Ukumbi wa Kimataifa (JNICC) uliopo Jijini humo.

Amesema kuwa Mkutano huo ulioandaliwa na Wizara hiyo kwa kushirikiana na Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) na wadau wa Sekta ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara, unatarajiwa kuwa na washiriki zaidi ya 500, lengo kuu ni kufanya majadiliano ya namna ya kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini kwa lengo la kukuza uchumi na kuchochea maendeleo ya Taifa.

“Hatua hii, inaakisi dhamira ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kukuza na kuimarisha majadiliano na ushirikiano kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi”

“Mkutano huo utakua na washiriki zaidi ya 500 ukijumuisha viongozi mbalimbali wa Serikali wakiwemo viongozi wakuu kutoka Serikali ya Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mawaziri wa kisekta, Makatibu Wakuu wa wizara za kisekta, wenyeviti wa kongani mbalimbali, wamiliki wa kampuni, wamiliki wa viwanda, vyama vya Sekta Binafsi, jumuiya za wafanyabiashara, wawekezaji, wafanyabiashara wadogo na wa kati, wakuu wa taasisi za serikali, watafiti wabobezi, watunga sera, washirika wa maendeleo na Asasi za Kiraia (AZAKI).” amesema Gugu.

Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa TNBC, Dkt. Godwill Wanga amesema kuwa suala la uboreshaji mazingira ya Biashara ni la umuhimu kwani kwa sasa uchumi wa nchi upo katika asilimia 5.2 ambapo lengo ni kufikia asilimia 8.

Ameongeza kuwa uchumi unapokua kuna faida kubwa kwa mtu mmoja mmoja, lakini pia Taifa kwa ujumla. Hivyo ni vyema kuboresha mazingira ya Biashara kwa njia mbalimbali ili kuweza kufikia malengo katika suala zima la uwekezaji.

Octavian Mshiu ni Mkurugenzi wa Bodi Kutoka TPSF, amesema kuwa Tanzania ni moja kati ya nchi 10 za Afrika ambazo mazingira yake ya Biashara yameboreshwa kutokana na uongozi mahiri wa Serikali ya awamu ya sita ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Aidha amesisitiza kuwa Sekta Binafsi inaunga mkono jitihada za Rais Samia na kwamba wapo bega kwa bega na Serikali yake  kwa kushirikiana na serikali kwenye mijadala mbalimbali kama hiyo. 

Previous articleHALMASHAURI ZOTE NCHINI ZIMETAKIWA KUANZISHA MIRADI YA UWEKEZAJI  ILI KUPANDISHA MAPATO.
Next articleTUIMARISHE ELIMU KWA WANANCHI JUU YA UMUHIMU WA CHANJO – PROF. MAKUBI
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here